19 Machi 2022 - 11:10
Rais wa Algeria: Jinai za Ufaransa nchini Algeria hazitasahaulika

Rais wa Algeria amelihutubia taifa kwa mnasaba wa maadhimisho ya uhuru wa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, wananchi wa Algeria hawatasahau jinai na uhalifu uliofanywa na Ufaransa huko humo.

Wanajeshi wa Ufaransa walipora maliasili za Algeria baada ya kuikoloni nchi hiyo kwa miaka mingi na kutekeleza jinai chungu nzima dhidi ya watu wa nchi hiyo. Algeria ilikoloniwa na Ufaransa kwa miaka 123.  

Zaidi ya Waalgeria milioni moja waliuliwa na wanajeshi wa Ufaransa katika kipindi cha vita vya kupigania ukombozi wa Algeria kuanzia mwaka 1954 hadi 1962.  

Shirika la habari la Mehr limeripoti kuwa, Rais Abdelmajid Tebboune wa Algeria jana Ijumaa alieleza kuwa, mkoloni Mfaransa hajailetea Algeria manufaa yoyote ghairi ya kuisababishia nchi hiyo uharibifu na maafa. Amesema, faili la jinai za Wafaransa nchini Algeria linapasa kuchunguzwa kwa haki na uwazi.  

Rais Tebboune aliwahi kukosoa na kulaani jinai zilizofanywa na Ufaransa huko Algeria na kueleza kuwa, ukoloni wa Ufaransa nchini kwake kuanzia mwaka 1830 hadi 1962 ulifanya uhalifu wa kutisha sana ambao haujashuhudiwa katika historia ya sasa ya mwanaadamu.

342/